Ibada hiyo takatifu ya Ekaristi ilifanyika siku ya Ijumaa, ikiwa ni tukio la kihistoria na la kipekee kwa Kanisa la Katoliki.
Katika homilia yake, iliyotolewa kwa lugha ya Kiitaliano, Askofu wa Roma aliwahimiza Wakristo duniani kote kushikamana kwa ajili ya Kanisa linalojikita katika Injili, kwa mujibu wa mapenzi ya Mungu. Alisisitiza haja ya kujenga madaraja ya matumaini, amani, na umoja – kama msingi wa maisha ya Kikristo leo.
Akinukuu maneno ya mtangulizi wake, Papa Francisko, aliwataka waumini kuishi imani ya kweli katika kila hali ya maisha, hasa katika nyakati hizi ngumu ambapo maovu yanazidi kuenea kwa kasi duniani.
“Uovu hautashinda,” alitangaza Baba Mtakatifu, akiwataka maaskofu kuendeleza ujumbe huo katika huduma yao, wakiwa kati ya marafiki wa Yesu waliowekwa wakfu kwa ajili ya kazi hiyo.
Papa mpya alihitimisha kwa kuomba nguvu ya Roho Mtakatifu na maombezi ya Bikira Maria, Mama wa Kanisa, ili awe mchungaji mwaminifu wa Kanisa la Ulimwengu, akizingatia kikamilifu Maandiko Matakatifu.
Katika mahubiri hayo, alielezea masikitiko yake juu ya kupungua kwa imani kunakosababishwa na kuweka pesa mbele kuliko kiroho, akisisitiza kuwa changamoto hizo za kiroho zinaweza kushindwa kupitia sala, mshikamano, na kuungana na waliodhulumiwa.
Kama ilivyokuwa kwa Papa Francisko, Papa Leon wa XIV aliweka wazi udhaifu wake wa kibinadamu, akibainisha kuwa sala na kujitoa kwa Bikira Maria ni msaada wa kweli anaouhitaji katika kila hatua ya utume wake wa kipapa. Alikumbusha pia kuwa utume wa Kitume anaochukua sasa unakumbwa na changamoto nyingi, lakini zote zinaweza kutatuliwa kwa njia ya maombi na ushirikiano wa kiroho.
Tarehe 8 Mei 2025, Kardinali Francis Prevost kutoka Marekani alichaguliwa kuwa Papa wa 267 wa Kanisa Katoliki, na kuchukua jina la Leon wa XIV. Akiwa na umri wa miaka 69, alichukua nafasi ya Papa Francisko aliyefariki dunia tarehe 21 Aprili 2025. Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa Mmarekani kuchaguliwa kushika wadhifa huo wa juu kabisa katika Kanisa.
Mzaliwa wa Chicago, Prevost ni mshiriki wa Shirika la Mtakatifu Augustino na alihudumu kwa muda mrefu kama mmisionari nchini Peru. Kabla ya uchaguzi wake, alikuwa akihudumu kama Mkuu wa Idara ya Maaskofu (Prefect wa Dicastère kwa ajili ya Maaskofu), nafasi ya juu yenye ushawishi mkubwa katika uongozi wa Kanisa Katoliki.
Anajulikana kwa kuzungumza lugha nyingi, unyenyekevu, moyo wa kichungaji, na utayari wa kuendesha mazungumzo yenye kujenga. Anaendelea kubeba urithi wa Papa Francisko kwa kusisitiza Kanisa linalojali watu, hasa walioko pembezoni, na lililo wazi kwa changamoto za kisasa.
Uchaguzi wake ulipokelewa kwa shangwe na viongozi mbalimbali duniani, kama ishara ya kuimarisha uasilia wa Kanisa na kuchukua mwelekeo wa kichungaji, jumuishi, na wenye kujali utu wa binadamu.
Mwishoni mwa Misa ya kwanza iliyoadhimishwa katika Kanisa la Sistine, Papa Leon wa XIV aliwabariki waumini kwa moyo wa shauku na roho ya ukaribu. Washiriki wote, wakiwemo makardinali, walimshangilia kwa makofi na furaha, katika ukimya wa sala uliotawala ibada hiyo ya pekee.