“Kuwa msema Kiswahili hakumkingi mtu dhidi ya mashitaka pale ambapo mambo hayakufanywa kama yalivyopaswa kufanywa,” alisema Muyaya mbele ya waandishi wa habari, huku akielekeza ujumbe wake kwa wale wanaoeneza tafsiri za kijimbo au kilugha kuhusu hatua za kisheria dhidi ya baadhi ya maafisa wa jeshi.
Kauli hiyo ya serikali inakuja wakati ambapo kumekuwa na ongezeko la mashitaka au uchunguzi dhidi ya baadhi ya maafisa wa jeshi walioko katika maeneo yenye mivutano ya kijeshi mashariki mwa DRC. Baadhi yao wanazungumza Kiswahili, lugha inayotumika sana katika majimbo ya Ituri, Kivu ya Kaskazini, Kivu ya Kusini, na Katanga.
Hali hiyo imechochea mijadala katika mitandao ya kijamii na hata matamko kutoka kwa baadhi ya viongozi wa kisiasa wa mashariki wakidai kwamba maafisa wao wanalengwa kimakusudi. Wengine walikwenda mbali na kuonya kuwa hali hiyo inaweza kuchochea mgawanyiko wa kitaifa na kutishia mshikamano wa kijeshi.
Muyaya, kwa niaba ya serikali, alisema kuwa ni hatari kubwa kuingiza siasa na ukanda katika masuala ya sheria na uwajibikaji. “Hii ni sumu. Sumu ya mgawanyiko. Tuna wajibu wa kuijiepusha. Tunapoanza kusema huyu anashitakiwa kwa sababu ni mswahilifoni, tunakuwa tunavunja msingi wa taifa moja,” alisema kwa msisitizo.
Aliwahakikishia wananchi kuwa mashitaka yanayoendelea si ya kulenga kundi fulani, bali ni sehemu ya juhudi za kujenga utawala wa sheria na kupambana na vitendo vya rushwa, uzembe wa kiutawala, na matumizi mabaya ya madaraka.
Wito kwa Umma na Vyombo vya Habari
Muyaya alitoa wito kwa viongozi wa kisiasa, asasi za kiraia, na vyombo vya habari kuwa waangalifu na matamko yanayoweza kueneza chuki au migawanyiko miongoni mwa wananchi. Alisisitiza kuwa badala ya kujenga hoja za kikanda, kila mtu anapaswa kusimama na kulinda haki, uwajibikaji na umoja wa kitaifa.
“Katika taifa linalojengwa juu ya misingi ya haki na usawa, tunahitaji kushikamana. Hatuwezi kuruhusu lugha au ukanda kuwa kigezo cha kuamua nani awajibike na nani asiulizwe maswali,” alihitimisha.
Kauli ya msemaji wa serikali inachukuliwa kama sehemu ya juhudi za serikali kuzuia mgawanyiko wa kitaifa unaoweza kutokana na tafsiri potofu za hatua za kisheria. Katika wakati ambapo DRC inapambana kurejesha amani mashariki na kuboresha taasisi zake za haki, umoja wa kitaifa unabaki kuwa silaha muhimu dhidi ya maadui wa ndani na wa nje.