Kwa moyo mzito na huzuni kuu, ninalazimika kusema ukweli. Ni vigumu kunyamaza kimya ninapoona jinsi taifa letu linavyoporomoka kwa kasi kubwa, si kwa sababu ya majanga ya asili au mashambulizi ya kigeni, bali kwa sababu ya uongozi usiojali, usio na maono, na usioheshimu dhamana ya taifa.
Miaka sita tu imepita tangu nilipoondoka madarakani, nikiliacha taifa likiwa na msingi thabiti wa amani, taasisi zilizojengwa kwa uangalifu, na matumaini ya kujenga mustakabali bora kwa kila raia. Leo hii, kwa masikitiko makubwa, naona urithi ule mzuri tukiwa tumegawana kama familia moja ya kitaifa, umeteketezwa kabisa na wale waliokabidhiwa kuutunza.
Taifa letu linatoa taswira ya kuvunja moyo, hali inayozua masikitiko makubwa kwa wananchi wa ndani, na kwa mataifa mengine, kuwa chanzo cha dhihaka, huruma na kejeli.
Ni aibu iliyoje, kwamba taifa lenye utajiri mkubwa wa madini, ardhi, mito, misitu na watu wenye akili na bidii, linaonekana leo dunia nzima kama mfano wa kushindwa. Na haya yote, si kwa sababu hatuwezi, bali kwa sababu ya uongozi usiojali na usiokuwa na uchungu na nchi hii.
Uongozi Bila Dira, Taifa Bila Mwelekeo
Tunashuhudia kila siku vitendo vya ubinafsi, uroho wa mali, ukabila wa waziwazi, na upendeleo wa kikundi kidogo chenye nguvu. Ahadi hazitekelezwi, sheria haziheshimiwi, na maisha ya raia wa kawaida hayathaminiwi.
Watu waliowahi kuamini katika mabadiliko sasa wamekata tamaa. Vijana, badala ya kuona fursa, wanaona kiza. Dunia, badala ya kutuheshimu, wanatucheka. Na yote haya yanatokana na kutowajibika kwa viongozi walioko madarakani.
Ni wazi kuwa hali ya sasa haiwezi kudumu. Hakuna taifa linaloweza kusimama juu ya msingi wa uongo, ubinafsi na uzembe. Bila mabadiliko ya kweli ya uongozi na mfumo mzima wa utawala, DRC itazidi kuyumba, na wananchi wake wataendelea kuteseka.
Wito wa Kusimama na Kutetea Taifa Letu
Naandika haya si kwa lengo la kulaumu tu, bali kwa lengo la kutoa wito wa kitaifa: fuungueni macho, tuamke, tuokoe nchi yetu.
Ni lazima turudi kwenye maadili ya msingi: Umoja, haki, uwajibikaji, na heshima kwa kila raia – bila kujali kabila au eneo. Ni lazima viongozi waelewe kuwa mamlaka ni dhamana, si fursa ya kujinufaisha.
Tukinyamaza sasa, historia haitatusamehe. Na zaidi ya historia, vizazi vijavyo vitatuhukumu kwa uzito mkubwa.
Tuache mzaha katika siasa. Tuache ubinafsi katika utumishi wa umma. Tuikomboe DRC kutoka kwenye lindi la aibu na umaskini uliochochewa na ubadhirifu.
Tutakapoangalia nyuma, je, tutasema tulichagua kunyamaza, au tutajivunia kuwa miongoni mwa walioinua sauti kwa ajili ya haki, umoja na mustakabali wa taifa letu?
Chaguo hilo ni letu – sasa.