Sababu kuu ya suluhisho hii ni pendekezo la upande wa waasi linalodai mamlaka ya kuendesha majimbo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini kama “entité autonome” kwa kipindi cha miaka minane.
Katika kujibu pendekezo hilo, Prince Epenge, msemaji wa muungano wa upinzani wa LAMUKA unaoongozwa na Martin Fayulu, alitoa tamko kali lililojaa ukosoaji wa wazi kwa serikali na wale anaowataja kama “washirika wa kigeni wanaotaka kuimega DRC vipande vipande.”
“Madai ya M23/AFC si wazimu wa kisiasa, bali ni tusi la moja kwa moja kwa historia ya ukombozi wa taifa letu. Lumumba alipigana na kufa kwa ajili ya Congo moja, sio vipande viwili vya Kivu vinavyotawaliwa na genge la waasi,” alisema Epenge.
Kwa mujibu wa vyanzo vya karibu na mazungumzo hayo, AFC/M23 imewasilisha masharti kadhaa, ikiwemo:
- Kuundwa kwa serikali ya mpito katika Kivu Kaskazini na Kusini, chini ya usimamizi wao;
- Kusitishwa kwa operesheni zote za kijeshi za FARDC na SADC katika maeneo yao ya udhibiti;
- Usimamizi wa mipaka ya mikoa hiyo kwa miaka 8, na fursa ya kujadili “uhuru wa kudumu” baadaye.
Katika muktadha huu, Epenge alielezea hofu ya LAMUKA kwamba mazungumzo ya Doha yamegeuka kuwa “mtego wa kisiasa wa kimataifa” unaolenga kuhalalisha ushindi wa kijeshi wa AFC/M23, kwa baraka za baadhi ya mataifa jirani.
“Hatutakubali hata kwa dakika moja Kivu kugeuka kuwa ‘cheo cha zawadi’ kwa wale waliotumia risasi na damu kujaribu kuhalalisha siasa chafu. Huu ni mwanzo wa Balkanisation – na tunaapa kupinga kwa gharama yoyote,” aliongeza.
Katika taarifa hiyo yenye mvutano mkubwa, Prince Epenge alimshambulia pia Denis Kadima Kazadi Nanga, ambaye ni mshirika wa karibu wa serikali na hivi sasa anatajwa kuwa mmoja wa washauri wa Rais Tshisekedi katika mchakato wa Doha.
“Mwambieni Nanga: unaweza kupinga udikteta bila kuuza ardhi yako. Aibu kubwa ni kuona wapambanaji wa jana wakigeuka mawakala wa mipango ya kishetani ya kugawa Congo,” alisema.
Kwa kumalizia, Epenge alimnukuu Albert Einstein akisema:
“Hakuna tatizo linaloweza kutatuliwa kwa kutumia kiwango kilekile cha fikra kilichokisababisha. Kama Félix Tshisekedi si suluhisho, basi Nanga na waliomuumba si suluhisho pia.”
Wakati mazungumzo yakiendelea kwa usiri mkubwa, baadhi ya vyanzo kutoka ndani ya ujumbe wa serikali vinasema kuna mgawanyiko mkubwa kati ya maafisa wa Kinshasa kuhusu namna ya kushughulikia masharti ya waasi. Wengine wanapendekeza “mkataba wa mpito kwa ajili ya amani,” huku wengine wakihofia kuwa hiyo ni njia ya kuhalalisha kutengwa kwa mikoa miwili muhimu ya nchi.
Kwa sasa, hali ya taharuki imeendelea kutanda nchini Congo, huku wananchi wengi wakiitazama Doha kama hatima ya mustakabali wa ardhi yao. Maandamano madogo yameripotiwa mjini Bukavu, Goma na Kisangani, huku viongozi wa kidini, wanaharakati na wazee wa jadi wakitoa wito wa umoja wa kitaifa kupinga “mpango wa kusaliti nchi.”
Hatua inayofuata?
Jicho la taifa sasa limeelekezwa Doha. Ikiwa serikali ya DRC itakubali hata sehemu ya madai ya waasi, basi upinzani unatishia kuanzisha mchakato wa “uasi wa kiraia,” ikiwa ni pamoja na maandamano makubwa, migomo na kampeni ya kukataa uhalali wa serikali ya Kinshasa.
Kwa wengi, Doha si tena jukwaa la mazungumzo ya amani bali ni jaribio la mwisho kuamua iwapo Congo itabaki moja au itaanza kutawanyika.