Kupitia ujumbe wake mfupi lakini mzito wa maana, Numbi alitowa mfano wa Jenerali Christian Tshiwewe, aliyekuwa Mkuu wa Majeshi, ambaye sasa anashutumiwa kuwa “adui wa taifa” bila ushahidi wowote.
Katika ujumbe huo, Jenerali Numbi aliandika:
“Tout se paie ici sur terre. Hier, militant de l’UDPS jusqu’à organiser des causeries morales pour se faire bien voir de l’autre côté, le Gén. Tshiwewe aujourd’hui est l’ennemi du pays sans preuve matérielle. Le créateur n’a pas peur de sa créature.”
(Kila kitu hulipwa hapa duniani. Jana, mwanaharakati wa UDPS hadi kuandaa mijadala ya maadili ili apate kuonekana vizuri upande wa pili, Jenerali Tshiwewe leo hii ni adui wa nchi bila ushahidi wa moja kwa moja. Muumba haogopi kiumbe chake.)
Kauli hiyo inakuja siku chache baada ya Jenerali Tshiwewe kutajwa katika taarifa za usalama kuwa ni mshukiwa mkuu wa njama ya mapinduzi ya kijeshi iliyodaiwa kudhibitiwa na vyombo vya usalama vya taifa. Hadi sasa, hakuna ushahidi wa wazi uliotolewa hadharani kuthibitisha madai hayo, jambo ambalo limeibua maswali kuhusu uwazi wa utawala wa sasa na uwepo wa mvutano ndani ya taasisi za kijeshi.
Jenerali Numbi, ambaye mwenyewe amewahi kukumbwa na tuhuma mbalimbali za kisiasa na kijeshi, anaonekana kutumia kauli hiyo kuonyesha unafiki na kigeugeu cha siasa za ndani ya UDPS na mfumo wa utawala wa sasa wa Rais Félix Tshisekedi.
Wachambuzi wa mambo ya siasa nchini wanasema kauli ya Numbi si tu ni ya kisiasa, bali pia ni onyo kwa wale wanaoamini kuwa kuwa karibu na mamlaka ni kinga ya milele. Wengine wanaona ni dalili za mgawanyiko mkubwa unaoendelea ndani ya uongozi wa kijeshi na kisiasa wa nchi.
Taarifa rasmi kutoka serikalini kuhusu hali ya Jenerali Tshiwewe bado hazijatolewa kwa kina, huku idara ya usalama ikiongeza ulinzi wake katika maeneo ya mkakati jijini Kinshasa.
Katika kipindi hiki kigumu cha kisiasa kwa DRC, ujumbe wa Numbi umetafsiriwa na wengi kuwa ni ukumbusho wa misingi ya haki, ukweli, na hatima ya kila mmoja mbele ya historia.